Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, katika ujumbe wake wa kupongeza kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zainab (s.a.) na Siku ya Wauguzi, alitoa shukrani na pongezi zake kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na wauguzi katika sekta ya afya.
Matini kamili ya ujumbe wa Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا
“Na mwenye kumwokoa mtu mmoja na mauti, ni kana kwamba amewaokoa watu wote.”
(Surat Al-Ma’idah, aya ya 32).
Wauguzi wetu wenye thamani kubwa na Malaika katika sekta ya afya!
Salamu na amani ya Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu, ninyi ambao mmeidhihirisha subira ya Zainab katika namna ya kuwahudumia waja wa Mwenyezi Mungu.
Kutengwa siku ya wauguzi ili iadhimishwe katika siku ya kuzaliwa Aqilah Bani Hashim, Bibi Zainab al-Kubra (s.a.), ni ushahidi bora kabisa wa uhusiano usioweza kutenganishwa kati ya “kuuguza mwili” na “kusimama imara katika kushikamana na tunu za juu na adhimu.”
Bibi huyo mtukufu hakuwa muuguzi wa Karbala pekee, bali pia alikuwa kinara wa msimamo thabiti na subira katika nyakati ngumu zaidi za historia. Nanyi leo ni waendelezaji wa njia hiyo hiyo ya kujitolea na kujitoa muhanga.
Hawza, kwa kuthamini juhudi zenu zisizokoma na kazi zenu za mchana na usiku, zinaichukulia siku hii yenye baraka kuwa fursa ya kutoa shukrani na pongezi kwa juhudi za dhati zinazofanywa na watu ambao, katika uwanja wa tiba, kwa upendo na imani, hupunguza maumivu ya wanaoteseka na kurejesha matumaini katika mwili wa jamii.
Ninyi si watu wanaopunguza maumivu ya miili iliyochoka pekee, bali pia, kupitia mwenendo wenu wenye huruma na staha, maadili yenu yenye utulivu na kuhifadhi heshima ya utu wa mwanadamu katika mazingira ya matibabu, mnakuwa waenezi wa vitendo wa mafundisho ya maadili ya Uislamu.
Fahamuni kwamba huduma hii ya dhati, inapopimwa katika mizani ya uadilifu wa Mwenyezi Mungu, ni ibada kubwa na jihadi adhimu ambayo thawabu yake itahifadhiwa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Mimi binafsi, sambamba na kuwapongeza kwa siku hii yenye furaha na baraka, ninamuomba Mwenyezi Mungu, Mwenye neema nyingi, awajalie wauguzi wote wenye kujitolea na wanaofanya kazi kwa bidii katika nchi yetu mafanikio yanayozidi kuongezeka, afya njema na endelevu, pamoja na kupata msaada na tawassuli kwa Bibi Zainab al-Kubra (s.a.) katika njia ya kuwahudumia viumbe Wake.
Natumaini kwamba kivuli cha fadhila na rehema za Mwenyezi Mungu kitaendelea kuwafunika ninyi pamoja na familia zenu zenye heshima daima.
Ayatullah Alireza A‘rafi
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran.
Maoni yako